Header Ads

Swali; kinzanisha Taaluma ya Isimu maana, Isimu Amali na Isimu Kokotozi.


SWALI:
Kinzanisha Taaluma ya Isimu maana, Isimu Amali na Isimu Kokotozi.

UTANGULIZI:
Maana ya Isimu:
Kwa mujibu wa TUKI, (2013).  Isimu ni taaluma inayochunguza na kuchambua lugha kisayansi.
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa Isimu ni Sayansi ya lugha inayochunguza au kushughulikia lugha za binadamu katika viwango mbalimbali  kiisimu kama vile fonetiki, fonolojia, semantiki, pragmatiki na mofolojia.
Kwa mujibu wa Fromkin na Rodman, (1988). Anasema kuwa Isimu maana ni uchunguzi wa maana ya maneno vishazi na sentensi katika lugha.
Kutokana na fasihi za wataalamu hao tunaweza kusema kuwa Isimu maana ni taaluma inayojihusisha na maana za maneno katika lugha.
Kwa mujibu wa Wanjala, (2011:99). Anaeleza kuwa Isimu amali ni ngazi ya Isimu inayochunguza amali na desturi za jamii fulani na namna zinavyoathiri matumizi ya lugha.  Huchunguza athari ya muktadha, desturi, tamaduni na vikwazo vya jamii mahsusi katika matumizi ya lugha wakati wa mawasiliano.  Isimu amali hujikita zaidi katika kuchambua kinachomaanishwa na mtoa ujumbe katika muktadha fulani wa kijamii na wala si maana ya kawaida ya neno au tungo.
Kwa mantiki hiyo ni dhahiri kuwa Isimu amali inajikita zaidi katika maana halisi aliyonayo mzunguzaji na si maana halisi ya neno.
Wanjala, (2011:154). Anaeleza kuwa Isimu kokotozi ni tawi mahuruti la isimu linaloshughulikia takwimu na kanuni za kufinyanga lugha kwa mtazamo mkokotoo.  Taaluma hii inajihusisha na tafsiri na ukalimani kupitia matumizi ya mashine na tarakilishi katika uhawilishaji wa ujumbe.
Hivyo basi Isimu Kokotozi ni taaluma inayotumia vifaa vya kisasa katika zoezi la kutafsiri na kukalimani matini mbalimbali kutoka Lugha chanzi kwenda Lugha lengwa, vifaa hivyo ni kama vile simu, tarakilishi (Computer).
Taaluma ya Isimu manaa, Isimu amali na Isimu kokotozi hukinzana katika namna mbalimbali kama ifuatavyo:
Ukinzani katika maana, hujitokeza kwa kuangalia maana ya kila taaluma, mfano katika taaluma ya Isimu maana, inajikita katika kushughulikia maana ya maneno, vishazi na sentensi katika lugha.  Wakati katika taaluma ya Isimu amali yenyewe inajikita katika amali na desturi za jamii fulani na namna zinavyoathiri matumizi ya jamii fulani, huchunguza athari ya muktadha, desturi na tamaduni za jamii fulani; taaluma hii hujikita zaidi katika kuchambua kinachomaanishwa na mtoa ujumbe na wala si maana halisi ya neno au maneno husika kama ilviyo kwa Isimu maana.
Mfano: Katika Isimu amali tunaweza kusema “Konda alimwambia dereva wake kuwa, nilikula vichwa vingi sana leo”.  Akiwa ana maana kuwa alipata abiria wengi sana siku hiyo.
Ila katika Isimu maana ambayo maneno huangaliwa kama yalivyo tunaweza kusema kuwa konda alikula vichwa vingi sana (kama kitendo cha kuweka mdomoni kutafuna na kumeza). Ila katika taaluma ya Isimu Kokotozi yenyewe, imejikita katika tafsiri na ukalimani kupitia matumizi ya mashine na tarakilishi katika uhawilishaji wa ujumbe, suala ambalo lenyewe linatofautiana kabisa na taaluma maana na amali.
Ukinzani katika viwango vya utendaji kazi (Wanjala, 2011). Isimu amali hujishughulisha katika masuala mbalimbali katika uchunguzi wake wa matumizi ya lugha katika mawasiliano, matumizi ya lugha kama ifuatavyo:
(i) Udhanalizo – Ni hali ya kuwa na ufahamu wa awali wa jambo linalotolewa na msemaji.
Mfano: Mjomba wangu amepata tena ajali.
Sentensi hii inatolewa na mtoaji na kueleweka kwa mlengwa kwa sababu tayari mlengwa anafahamu kwamba mtoa ujumbe ana mjomba wake pia alishawahi kupata ajali.
(ii) Vimanilizi vya mawasiliano – Ni maana nyingine anayoipata mlengwa baada ya kupokea ujumbe au usemi kutoka kwa msemaji.
Mfano: Umeshauona mchana? Hapa maana rejewa ni je, umeshapata chakula cha mchana na wala si kushuhudia mchana ukiingia.
(iii) Uchopezi – Ni sentensi zinazotoa maafikiano kutokana na mantiki, yaani sentensi ya kwanza inasaidia sentensi ya pili kuwa ya kweli au ya uongo.
Kwa mfano:
Neema ni mkristo na wala si mwislamu.
Neema amelipa mahari.
Neema ametoa zaka.
Padre Deus alifungisha ndoa ya Neema.
(iv) Uolezi – Ni urejeleaji au uhusanishaji wa kitajwa na kitaja kaitka muktadha wa washiriki wa mawasiliano.  Viashiria hivi hutumiwa kubainisha nafsi, njeo na mahali.
Kwa mfano:
Mchungaji yupo anahubiri.
Yupo ni kiolezi kinachoashiria mahali ambapo Mchungaji anahubiria inaweza ikawa kanisani au sehemu yoyote ile.
(v) Kanuni ya ushirikiano – humhitaji msemaji kusema kwa umakini na kwa kujiepusha na usemaji wa kutoeleweka ili kujenga maana inayokusudiwa.  Kanuni hii huwa na sifa mbalimbali kama vile idadi, namna, hiari, ubora, uhusiano na ukweli.
Kwa mfano:
Nilikwenda nikamkuta hayupo.
Sentensi hii inakiuka kanuni za ushirikiano kwani mtu hawezi ukamkuta na wakati huo huo, akawa hayupo.
Ilitakiwa tuseme hivi, nilipoenda kwake sikumkuta.
(vi) Enthnografia ya mawasiliano – huchunguza iwapo tukio la mawasiliano limeafiki lengo lake au la.  Huchunguza hali, mpangilio na kazi ya mazungumzo kwa mujibu wa mila na tamaduni za jamii husika.  Na huzingatia kaida za mazungumzo ambazo ni muktadha, wakati pamoja na vitendo.
Kwa maana hizo hapo juu ni dhahiri kuwa utendaji kazi katika Isimu amali umegawanyika katika viwango, wakati viwango vya utendaji  kazi katika Isimu maana ambayo yenyewe hujishughulisha na maana za maneno, vishanzi na sentensi katika lugha. Katika kiwango cha sentensi tunatumia sifa za kiarudhi yaani Shadha au Kiimbo ili kubainisha maana husika.
Kwa mfano: (i) Unakula nini? (Kuuliza).
(ii) Toka nje (Amri).
Katika kiwango cha neno tunatumia sifa ya kiarudhi ya mkazo kubainisha maana ya neno.
Mfano: Taˋbia, `kaa, `pia.
Taaluma ya Isimu kokotozi (Computational linguistic) huhusisha utumiaji wa mashine na tarakilishi ambazo huwasilisha utumiaji wa mashine na tarakishi ambazo huzalisha aina mbili za uhawilishaji wa ujumbe ambao ni:
(i) Tafsiri mashine ambayo ni tawi la Isimu kokotozi linalochunguza matumizi ya violwa laini vya tarakishi katika  kuhawilishi ujumbe.  Tafsiri ya mashine hubadilisha maneno katika lugha chasili kwa maneno sawia katika lugha lengwa.
(ii) Tafsiri tarakilishi: Ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri hutumia violwa laini vya tarakilishi katika kufasiri matini husika, ni uhawilishaji wa ujumbe unaoshirikisha binadamu ana saidiwa na tarakishi.  Hivyo basi mfasiri mkuu ni binadamu ila tarakilishi  inamsaidia tu kuboresha kazi yake, uhakiki huu hufanywa kwa kutumia violwa laini kama vile:
- Language search engine soft ware.
- Project management soft ware.
- File maker programme.
- Termilogy bank.
Ukinzani katika umri: Katika suala la umri sisi kama wanakikundi tunaona kuwa taaluma ya Isimu amali na Isimu maana zinaonekana kuwa kongwe zaidi ikilinganishwa na taaluma ya Isimu kokotozi ambayo imeibuka kutokana na kuwepo kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia kwani taaluma hii hutumia vifaa kama simu na tarakilishi katika kufikisha ujumbe.
Pia Ukinzani unaweza kujitokeza katika suala la gharama, kwani katika taaluma ya Isimu kokotozi inaonekana kuwa na gharama zaidi kuliko taaluma zingine, pia katika Isimu kokotozi ambayo hujishughulisha na utafsiri na ukalimani kupitia vyombo mbalimbali vya gharama kama simu, tarakilishi pamoja na mashine mbalimbali ambazo huhitajia gharama mbalimbali.
Ukinzani katika wahusika, katika Isimu kokotozi wahusika wake ni wale wenye ujuzi wa kutumia mashine mbalimbali, kama wanahisabati na wanatarakilishi tofauti na taaluma zingine kama Isimu maana na Isimu amali.

HITIMISHO:
Hivyo basi pamoja na ukinzani uliopo baina ya taaluma hizi yaani Isimu amali, Isimu maana na Isimu Kokotozi ni dhahiri kuwa taaluma hizi huenda pamoja katika suala zima la utafsiri na ukalimani.  Kwani zinahusiana kwa kiasi kikubwa katika kuhawilisha ujumbe.

MAREJELEO:
Fromkiri, V and Rodrean, R. (1988). An Introduction to Language. Fort North: Holt Rinehart and Wriston Inc.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu, (2013). TUKI: Oxford University Press, East Africa Ltd. Kenya.
Wanjala, S. (2011). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri. Mwanza, Tanzania: Serengeti Educational Publishers (T) Ltd.


4 comments:

Powered by Blogger.