Header Ads

DHANA YA URADIDI KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI


UTANGULIZI
Dhana ya uradidi,
Kwa mujibu wa Rubanza (1996), anafasili uradidi kuwa ni njia ya kuunda maneno mapya katika Kiswahili, kama ilivyo katika lugha zingine ni kurudufu au kwa maneno mengine ni kurudia maneno. Neno lote zima linarudiwa au sehemu ya neno linarudiwa. Linaporudiwa neno zima kitendo hicho huitwa urudufu kamili na linaporudiwa sehemu ya neno ni urudufu nusu.

Kwa mujibu wa Matinde (2012), uradidi ni utaratibu unaotumika katika kuunda maneno ambayo sehemu ya neno lote hurudiwa na kuunda neno au msisitizo fulani.
Fasili ya Matinde ina upungufu katika kufasili hasa nini maana ya uradidi kwani si lazima neno lote lirudiwe, huweza kuwa sehemu tu ya neno.

Hivyo tunaweza kusema kuwa uradidi ni kanuni au utaratibu katika lugha wa kuunda neno/maneno mapya kwa namna ya kurudia sehemu ya neno au neno zima. Ili hali sehemu ya neno ikirudiwa huitwa urudufu nusu na ikiwa ni sehemu nzima ya neno hujulikana kama urudufu kamili.
Mfano,
Nungu + nungu =    Nungunungu
Pilika + pilika     =   Pilikapilika
Kizungu + zungu =  Kizunguzungu
Kimbele + mbele =  Kimbelembele

Aina za uradidi.
Kuna aina mbili za uradidi kutokana na namna ambavyo neno hurudiwa. Aina hizo ni:
(i)                 Uradidi kamili
(ii)               Uradidi nusu

Uradidi kamili,
Rubanza (1996), anafasili kuwa uradidi kamili ni aina ya uradidi ambayo kwayo ni neno zima hurudiwa ili kuunda neno moja. Na hicho kitendo huitwa uradidi kamili.

Massamba (2009), anafasili kuwa uradidi kamili (complete reduplication) ni uradidi ambapo neno lote hurudiwa.
Kwa mfano,
            Kanuni: Neno + neno =          Neno jipya.
                         Peta + peta   =            petapeta
                        Pole + pole   =             polepole
                        Haraka  + haraka  =     harakaharaka
                        Cheka + cheka  =        chekacheka
                        Pilika + pilika =           pilikapilika
                        Pika  + pika =              pikapika
                        Shamra + shamra   =   shamrashamra
                        Cheza  +  cheza  =       chezacheza
                        Kimbia  + kimbia  =    kimbiakimbia

Uradidi nusu,
Kwa mujibu wa Rubanza (1996), anaeleza kuwa uradidi nusu ni aina ya uradidi katika uundaji wa maneno ambayo kwayo sehemu ya neno hurudiwa ili kuunda neno jipya/ maneno mapya katika lugha. Hali hii hujulikana kama urudufu nusu.

Massamba (2009), anafafanua kuwa uradidi nusu (partial reduplication) ni uradidi ambao kwao sehemu tu ya neno hurudiwa, kwa mfano: pepeta.
 Hivyo maneno hayo hurudiwa kwa madhumuni ya kutilia msistizo au hali fulani.
Kwa mfano:
            Ki + zungu + zungu    = kizunguzungu
            Ki + wili + wili =           kiwiliwili
            Ki + nyume + nyume = kinyumenyume
            Ki + nyevu + nyevu    = kinyevunyevu
            Ki + mbele + mbele     = kimbelembele
Katika mifano hiyo tumeona uambatanishaji wa mofimu tatu, yaani mofimu {ki-} na mofimu huru mbili. Kiambishi awali {ki-} kinadondoshwa katika neno la pili.
Kanuni: {ki} +{m-huru} + {m-huru} = Neno.

Dhana ya uambatanishaji.
Matinde (2012), anadai kuwa uambatanishaji ni mbinu ambayo huhusisha kuunganishwa kwa maneno mawili kuunda neno moja jipya ambalo maana yake huwa tofauti na maneno ambayo yametumika kuunda neno hilo.
Rubanza (1996), anaeleza kuwa uambatanishaji ni dhana ihusuyo uwekaji pamoja wa maneno mawili au zaidi ili kuunda neno moja. Uambatanishaji, badala ya kunyumbua mofimu katika mzizi sasa tunaweka maneno mawili au zaidi pamoja. Maneno hayo yanaweza kuwa huru au kuambatanishwa na kunyambulishwa na mofimu.

Hivyo tunaweza kusema kuwa, uambatanishaji ni kanuni au taratibu ihusuyo uundaji wa maneno mapya katika lugha kwa namna ya kuunganisha maneno mawili tofauti na kuunda neno moja. Uunganishaji huo wa maneno huweza kuwa ya kategoria moja au kategoria tofauti.
Mfano:
Nomino + nomino
            Mwana + siasa  = mwanasiasa
            Bata + mzinga  = batamzinga
           Mwana + jeshi  = mwanajeshi
           Njugu + mawe = njugumawe
           Askari + kanzu = askari kanzu

Nomino + kivumishi
               Pembe + kali =         pembekali
               Mwana + haramu =  mwanaharamu
               Mwana + mkaidi =   mwanamkaidi
               Mja + mzito  =         mjamzito
               Mbuzi + jike =         mbuzi jike
Kitenzi + nomino
           Piga + mbizi =     pigambizi
           Pima + maji  =      pimamaji
           Chemsha + bongo = chemshabongo
            Zima + moto =     zimamoto

Nomino + kitenzi
            Bongo + lala =            bongolala
            Nyama + choma =    nyama choma
Kitenzi + kielezi
            Ona + mbali =         onambali

HITIMISHO
Njia hizi mbili za uundaji wa maneno hazina tofauti kubwa,tofauti iliyopo ni kuwa  katika uambatanishaji maneno mawili tofauti yanaunganishwa pamoja. Matendo haya mawili ya uambatanishaji na uradidi yana msingi mmoja ulio sawa. Maana ya neno mojamoja hailingani na maana ya maneno mawili yanapoungwa pamoja.


 MAREJELEO.
Massamba, D. P.B (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar-Es Salaam: Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati          na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Rubanza, Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar-Es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha      Tanzania.



4 comments:

Powered by Blogger.