Header Ads

DHANA YA UUNDAJI WA MANENO:

UTANGULIZI:
Uundaji wa maneno ni mabadiliko ya istilahi na muundo unaosababishwa na mabadiliko ya sayansi na tekinolojia katika Nyanja mbalimbali za jamii ili kukidhi dhima ya lugha kama chombo kinachojitosheleza katika mawasiliano. Ili kukidhi haja hii kuna mbinu mbalimbali zinazotumika katika uundaji na ukuzaji wa istilahi ya maneno katika lugha. (Matinde 2012:110).

Hivyo basi uundaji wa maneno ni ujenzi au uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya. Uundaji wa maneno mapya husaidia kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano. Uundaji wa maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii. Kwa mfano tunayo maneno mapya kama vile ufisadi, uwekezaji, ujasiriamali, ukeketaji na mengine mengi kutokana na mabadiliko ya kijamii.
Zifuatazo ni mojawapo ya njia za uundajia wa maneno katika lugha ya Kiswahili:-

       I.             UTOHOZI:
Ni mbinu ambayo maneno kutoka lugha chanzi hutoholewa toka lugha chanzi na hatimaye hufanyiwa marekebisho kwa kufuata kaida au sheria za kifonolojia na kimofolojia za lugha pokezi kabla ya kutumiwa. Neno linapotoholewa hutamkwa na kuandikwa kwa utaratibu wa lugha pokezi,  hata hivyo maana ya neno lililotoholewa hubakia ileile ya awali. Matinde, (2012 :114).
Mifano:
KIINGEREZA
KISWAHILI
Switch
Swichi
Lorry
Lori
Budget
Bajeti
Agenda
Ajenda
Biology
Baolojia
Dollar
Dola
Oxygen
Oksijeni


 Ubora wa mbinu hii:
i)                    Mbinu hii ya utohozi ni mbinu rahisi ya kutumiwa katika uundaji wa msamiati. Mzungumzaji yeyote anaweza kutumia mbinu hii hata bila kuhudhuria kozi yoyote ya isimu au kufundishwa.
ii)                  Maneno mengi huweza kuundwa kwa kutumia mbinu hii ili kukidhi mahitaji ya matumizi katika lugha mbalimbali.

Udhaifu wa mbinu hii.
i)                    Mbinu hii hulemaza ubunifu wa wanajamii katika kuunda msamiati mpya wenye kuakisi utamaduni wa jamii husika.
ii)                  Lugha tohoaji huonekana kukosa uasilia yaani lugha huonekana kuwa chotara.
iii)                Baadhi ya maneno katika Kiswahili ambayo yametoholewa kutoka lugha ya kiingereza katika lugha ya Kiswahili hutamkwa kwa namna tofauti kabisa.
Mifano;
KIINGEREZA
KISWAHILI
Data
Data, deta
Dance
Densi, dansi
Bank
Bank, benki
Radio
Redio, radio

Hivyo basi, kutohoa maneno toka lugha nyingine ni ile hali ya lugha fulani kuchukua maneno toka lugha nyingine yaani kila lugha ina tabia ya kuchukua maneno toka lugha nyingine ili kukidhi mahitaji ya msamiati.

Maneno kutoka lugha nyingine yanapotoholewa hubadilishwa kimatamshi ili yafuate kanuni za lugha husika.
Katika lugha ya Kiswahili maneno yanayotoholewa hayana budi kusanifishwa na baraza la Kiswahili la Taifa ndipo yaruhusiwe kutumiwa rasmi.
Mifano mingine ya maneno yaliyotoholewa kutoka lugha nyingine ni kama ifuatayo:-
Dukani                        kihindi
Salamu                        kiarabu
Kitivo                          (kipare)
Ikulu                            (kigogo/kisukuma).
Bunge                          (kigogo).
    II.             TAFSIRI.
Matinde, (2012) anadai tafsiri ni mbinu ya kuunda maneno ambapo maneno au vifungu katika lugha chanzi hufasiriwa katika lugha lengwa. Ufasiri huu huzingatia muundo wa lugha pokezi.
Mifano,
KIINGEREZA
KISWAHILI
Free market
Soko huria
Ruling part
Chama tawala

Ubora wa mbinu hii.
Mbinu hii huzingatia kigezo cha maana zaidi kuliko muundo wa maneno yaliyochukuliwa toka lugha chanzi na kutafsiriwa huafiki utamaduni wa lugha lengwa. Hali hii husaidia katika kuunda maneno yenye maana iliyo wazi na inayokubalika katika lugha lengwa.

Udhaifu wa mbinu hii.
Mara nyingi huwa vigumu kutafsiri baadhi ya manenotoka lugha chanzi kwa kufuata kigezo maana.
Kuna uwezekano wa kupata tafsiri ambazo hazina maana wala mantiki katika lugha lengwa.
Mfano.
Kitchen party  -    sherehe ya jikoni.
Things fall apart  -   vitu vilivyoanguka na kutapakaa.

 III.            UFUPISHAJI:
Rubanza (1996) anaeleza kuwa baadhi ya majina ya maneno katika lugha nyingine za dunia hutokana na ufupishaji wa maneno yanavyotumiwa kwa pamoja kwa kutumia herufi au silabi za mwanzo tu za maneno hayo. Njia hii ameita Akronimu.
Matinde (2012) anaeleza kuwa ufupishaji ni mbinu ambayo hutokana na kitenzi ‘fupisha’ chenye maana ya kufanya kitu kiwe kifupi au kupunguza urefu wa kitu.
Kwa mujibu wa Rubanza (1996) njia ya ufupishaji imegawanyika katika sehemu kuu mbili kama ifuatavyo:-


a.      Akronomi.
Kwa mfano katika Kiswahili tuna maneno ambayo yametokana na herufi au silabi za mwanzo za maneno kama vile:-
UKIMWI        -           Ukosefu wa Kinga Mwilini.
TUKI              -           Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
BAKITA         -           Baraza la Kiswahili Tanzania.
TAKUKURU -           Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
KKKT             -           Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.

b.      Uhurutishaji.
Uhurutishaji ni tendo jingine linalokaribiana na tendo la akronimi, katika tendo hili vijisehemu vya maneno huwekwa pamoja kuunda neno jipya. Mfano katika lugha ya Kiswahili tunaweza kupata maneno kama vile:-
Chakula cha jioni    -               Chajio.
Hati za kukataza      -              Hataza.
Mama mdogo           -              Mamdo.
Chakula cha mchana -             Chamcha.
Vijisehemu vilivyowekwa pamoja si lazima viwe vyanzo vya maneno.

c.       Ufupishaji Mkato (clipping).
Matinde, (2012) anatofautiana na Rubanza (1996) kwa kuongeza mbinu nyingine ya ufupishaji ambayo ni ufupisho mkato (clipping). Katika mbinu hii baadhi ya vipashio au silabi hudondoshwa na kuacha sehemu tu ya neno asilia.
Mifano.
NENO ASILIA
KIFUPISHO
Dar es salaam
Dar
Shemeji
Shem
Morogoro
Moro
Dada
Da
Binamu
Bina



 IV.            KUINGIZA MANENO YA LAHAJA NA LUGHA ZA KIBANTU.
Hiki ni chanzo kingine cha upatikanaji wa istilahi za Kiswahili.

Dhana ya Lahaja.
Lahaja ni namna tofautitofauti  za kuzungumza lugha moja. Aina hizi tofauti za kuzungumza lugha moja haziwazuii wazungumzaji kuelewana. Mgulu, (1999:17).

a.        Kuingiza maneno kutoka lahaja za Kiswahili.
Mifano.
Wawe             -           kipate au kiamu
Mbolezi           -           kimvita.
Tungomsele     -           kiamu

b.      Kuchukua kutoka lugha nyingine za kibantu.
Njia ya kuchukua istilahi kutoka lugha ya kibantu imekuwa ikitumika kuongeza istilahi za Kiswahili.
Mifano.
Ngeli   -           Kihaya
Bunge -           kigogo
Ikulu    -           kisukuma

    V.            KUBUNI.
Matinde (2012) anasema ubunifu ni mbinu ya kubuni msamiati katika lugha husika na kurejelea dhana au vitu vipya ambavyo hapo awali havikuwepo katika jamii husika. Ni mbinu ambayo hutumiwa badala ya kuchukua maneno kutoka lugha nyingine. Mfano kubuni kwa kuongozwa na vigezo maalum kama ifuatavyo:-

Uakisi wa umbo la kirejelewa.
Kuna leksia za Kiswahili ambazo huakisi umbo la kiashiriwa.
Mifano ya maneno.
Neno ̔ Nyoka’ huibua taswira ya kitu kilichonyooka.
Neno ‘pembe kali’ hurejerea umbo lenye pembe iliyo na digrii pungufu ya 90.
Neno ‘kidole tumbo’ (appendix) huakisi umbo la sehemu ya mwili inayorejelewa ambayo ni kifuko  kama kidole ambacho kipo sehemu ya chini ya utumbo mkubwa.


Uakisi wa sauti au mlio.
Uakisi huu hubainika pale ambapo leksia huhusika kudhihirisha mfanano wa kisauti au mlio baina yake na kirejerewa.
Mifano.
Pikipiki            mlio, pik… pik… pik…
Kuku               mlio, ku… ku… ku…ku…
Cherehani        mlio, cherr…cherr…cherr…cherrr…

Uakisi wa tabia.
Baadhi ya leksia katika lugha huakisi tabia za kirejelewa, kwa mfano neno ‘Kifaurongo’ ambalo limeundwa kutokana na maneno mawili ‘kufa’ na ‘urongo’. Huyu ni mdudu apatiakanaye kwenye kokwa la embe ambaye akiguswa hujikunja na kukaa kimya kama amekufa. Hivyo basi neno kifaurongo huakisi tabia ya mdudu huyo.
Mfano mwingine ni ‘kinukamito’ ambayo imeundwa na maneno mawili ‘nuka’ na ‘mto’ hurejelea mtu anayeoa na kuacha  mara kwa mara (asiye na msimamo).

HITIMISHO:
Kwa ujumla uundaji wa maneno hupanua mipaka yake ya matumizi kwa kuongeza msamiati. Lugha nyingi ikiwemo lugha ya Kiswahili hutohoa baadhi ya msamiati kutoka lugha nyingine za dunia kutokana na mwingiliano wa watu. Lakini hata bila kutohoa maneno kutoka lugha nyinginezo kila lugha ikiwa pamoja na lugha ya Kiswahili kuna njia mbalimbali zzitumikazo katika kukuza msamiati wake.



                                                   MAREJELEO.
Masebo, J. A. (2010). Nadhari ya Lugha Kiswahili 1.Dar-Es Salaam: Nyambari Nyangwine
Publisher.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na
Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi
Kenya: Longhorn Publishers.
Rubanza,Y. I.(1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar-Es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.


10 comments:

  1. You have not answered my question please follow instructions

    ReplyDelete
  2. Naomba unielezee kuhusu udhaifu na ubora wa:ufupishaji na kubuni,kama mbinu zinazotumika katika uundaji wa maneno katika kiswahili

    ReplyDelete
  3. Naomba unielezee kuhusu udhaifu na ubora wa:ufupishaji na kubuni,kama mbinu zinazotumika katika uundaji wa maneno katika kiswahili

    ReplyDelete
  4. naomba unieleze sababu za uundaji wa maneno

    ReplyDelete

Powered by Blogger.